“Mimi ni Mtumishi wa Bwana na Nitendewe Kama Ulivyonena Bwana”
Written by ReganK on August 18, 2020
Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la DAR ES SALAAM Mhashamu YUDA THADEUS RUWAICHI amesema kuwa jibu la Mama BIKRA MARIA la mimi ni mtumishi wa Bwana na nitendewe Kama ulivyonena Bwana ni jibu la kila mkristo mbatizwa.
Askofu Mkuu RUWAICHI amesema hayo kwenye Adhimisho la Sadaka ya Misa Takatifu ya Jubilei ya fedha ya Upadre kwa mapadre nane wa Shirika la ndugu Wakapuchini iliyoadhimishwa jana katika Parokia ya BIKIRA MARIA Mama wa FATIMA MSIMBAZI Jimbo Kuu Katoliki la DAR ES SALAAM.
Amesema kuwa jibu la Mama BIKIRA MARIA ni jibu ambalo linapaswa kujibiwa na kila Mbatizwa, hivyo waliotimiza miaka 25 ya upadre wanapaswa kuendelea kulitoa jibu hilo ambalo walianza kulitoa siku ya ubatizo wao, siku ya nadhiri zao za kitawa na sasa waendelee kulitoa kwa uaminifu na udumifu hadi mwisho.
Wakati huo huo Askofu Mkuu RUWAICHI amewataka Mapadre walioadhimisha Jubilei ya miaka 25 ya upadre kutambua kuwa wao ni mashahidi wa habari njema, wajumbe na wanatumwa kuzitangaza sifa za Mungu, na kuutukuza wema na ukuu wake.
Mapadre walioadhimisha Jubilei ya miaka 25 ni pamoja na Mapadre SITA ambao ni Ndugu KALIST tesha Mkuu wa Shirika, Ndugu CYRIL NJAU, Ndugu AMBROCE MOSHA, Ndugu JOHN BOSCO MOSHA, Ndugu TITUS TARIMO, Ndugu GASTON KATEULE, Ndugu MARCUS MNUNDUMA na Ndugu FRANSIS LIRANGEZA.