Leo tutafakari tendo la kwanza la uchungu ambalo ni Yesu anatoka jasho la damu.
Kadiri ya Injili, baada ya Yesu kuweka Ekaristi Takatifu kwenye karamu ya mwisho, alikwenda kuanza rasmi mateso yake katika bustani ya Getsemani. Dhambi iliingia katika bustani ya Eden na mateso yatakayoondoa dhambi yanaanza katika bustani ya Getsemani.
Yesu alionekana mwenye hofu, mahangaiko na uchungu mkali. (Marko 14:32-34). Kwa nini Mungu awe katika hali hii? Yesu ni Mungu kweli lakini pia ni mtu kweli.
Yesu alikubali kubeba dhambi za ulimwengu hivyo alikubali pia kubeba matokeo ya dhambi katika ubinadamu wake. Matokeo ya dhambi ni hofu, mahangaiko, shida, uchungu na mashaka kutaja kwa uchache. Yesu anayapokea haya yote pale bustanini.
Kwa sababu ya dhambi kifo kiliingia duniani. Kifo kinatisha. Yesu anashiriki ubinadamu wetu kikamilifu ikiwa ni pamoja na kukipokea kifo.
Katika ubinadamu wake anapokaribia mateso na kifo anasali kuomba kama inawezekana saa hiyo impitie mbali. Lakini haraka haraka anasisiyiza kuwa mapenzi ya Mungu ndio yatimizwe. (Marko 14:35-36)
Yesu akiwa katika mahangaiko hayo anasali kwa bidii zaidi na anawataka mitume wake wasali pia lakini wanasinzia. Anataka kuwaambia kwamba katika shida kubwa na mahangaiko watafute nguvu katika sala. Hawamuelewi, hawakuweza kukesha hata kwa saa moja.
Kadiri ya mwinjili Matayo, Yesu alisali mara tatu akitumia maneno yale yale kuomba kama inawezekana kikombe kimuepuke lakini mapenzi ya Mungu ndio yatimie sio yake.
Mungu anaisikiliza sala ya Yesu lakini hamuondolei kikombe cha mateso na kifo. Anaisikiliza kwa kumpa nguvu ya kupokea mateso yaliyokuwa mbele yake. Malaika anakuja kumuimarisha. (Luka 22 : 43-44).
Akiwa katika mahangaiko hayo jasho la damu linatiririka usoni hadi ardhini. Labda kuondoa laana iliyowekwa katika ardhi kwa kosa la Adamu (Mwanzo 3:17).
Yesu akiwa katika mahangaiko hayo, Yuda anakuja na kikosi cha maaskari kumkamata.
Kwa muhtasari ni kwamba Yesu aliteseka na kuhuzunika pale Getsemani kwa namna alivyoyaona mateso yanayomkabili …….